Iran imesema iko tayari kuanzisha mazungumzo na Marekani, ikiwa tu mazingira yataruhusu kufanyika kwa mazungumzo hayo bila vitisho au shinikizo, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ameeleza.

Rais huyo amesisitiza kuwa mazungumzo hayo yatafanyika baada ya maombi kutoka kwa "serikali rafiki katika eneo hilo" na yatazingatia maslahi ya taifa.

Pezeshkian amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi, kushughulikia pendekezo la Marekani baada ya maombi kutoka kwa baadhi ya serikali za kikanda. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika Istanbuli siku ya Ijumaa, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuishambulia Iran katika maeneo yake ya nyuklia kufuatia ukandamizaji mbaya dhidi ya waandamanaji. Rais Trump amesema kuwa ingekuwa “vizuri” kama makubaliano yatapatikana, lakini pia ametahadharisha kwamba “matatizo makubwa” yatajitokeza kama mazungumzo hayatafanikiwa. Marekani imeongeza uwepo wa majeshi yake karibu na mipaka ya Iran, ikiwa ni pamoja na meli ya kivita USS Abraham Lincoln yenye ndege zaidi ya 70.

Hali ya ndani ya Iran imezidi kuwa tete baada ya maandamano makubwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana, yaliyochochewa na matatizo ya kiuchumi na matakwa ya mabadiliko ya kisiasa. Mashirika ya haki za binadamu yameripoti idadi kubwa ya vifo, ikiwemo watoto na baadhi ya watu waliokuwa na uhusiano na serikali.

Vyanzo vya habari vinabainisha kuwa uchunguzi kuhusu visa vya vifo unendelea, huku serikali ikitaja idadi rasmi ya waliokufa kuwa ndogo kuliko makadirio ya mashirika ya haki za binadamu