

Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameukaribisha Umoja wa
Vyombo vya Habari vya Mitandao ya Kijamii Mkoa wa Dodoma (UMIKIDO) na
kuutaka kuwa chachu ya kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na
wananchi kupitia utoaji sahihi wa taarifa pamoja na ubunifu wa maudhui.
RC
Senyamule ametoa kauli hiyo leo Februari 9, 2026, mara baada ya
viongozi wa UMIKIDO kufika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na
kuomba ushirikiano na Serikali ya Mkoa wa Dodoma.
“Hongereni
kwa kuanzisha umoja huu. Nimefurahishwa sana kwani utarahisisha kazi na
kuwa kiunganishi muhimu kati ya Serikali ya Mkoa na vyombo vya habari
vya mitandaoni. Tulitamani kupata watu wanaozungumza lugha moja na
Serikali, na tunaamini ninyi ni wazalendo,” amesema Mhe. Senyamule.
Ameeleza
kuwa uwepo wa umoja huo utaisaidia Serikali kufikisha taarifa kwa
wananchi kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuongeza uelewa wa umma kuhusu
shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa.
“Ni muhimu Watanzania wakaendelea kufahamu
kazi zinazofanywa na Serikali. Nina imani mtakuwa wabunifu katika
kuandaa na kusambaza taarifa kwa njia zitakazowafikia wananchi kwa
urahisi,” ameongeza.
Aidha,
RC Senyamule amewataka wanachama wa UMIKIDO kuzingatia kutangaza miradi
ya kimkakati na mipango ya maendeleo, ikiwemo uhifadhi wa mazingira,
matumizi ya nishati safi ya kupikia, sekta ya utalii na michezo, pamoja
na kuhamasisha matukio mbalimbali kuelekea mashindano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Awali, viongozi wa UMIKIDO
walieleza dhamira na malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo, ikiwa ni
pamoja na kuimarisha maadili ya uandishi wa habari za mitandaoni na
kushirikiana kwa karibu na Serikali katika utoaji wa taarifa sahihi kwa
umma. Pia waliomba ushirikiano kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutimiza
malengo hayo.
Viongozi walioshiriki ziara hiyo ni (Mwenyekiti wa
UMIKIDO Bw.Benny Majata,Katibu Emmanuel Charles, Zena Chitwanga
(Mhasibu), Daniel Mkate (Afisa Mahusiano), Alex Sonna (Kamati ya
Ufuatiliaji), Henry Masanja (Kamati ya Nidhamu) na Ronald Sonyo (Kamati
ya Fedha na Mipango).
Tunapatikana Kupitia