Morogoro, Februari 24, 2026 – Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limethibitisha vifo vya watu wawili vilivyotokana na athari za mvua, kufuatia kupigwa na radi katika Kitongoji cha Mbesi, kata ya Utengule, Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, tukio hilo lilitokea Februari 23, 2026 majira ya usiku wakati waathirika walikuwa wakirejea nyumbani wakitokea matembezini.

Waliofariki dunia ni Tano Leonard Lunasi (36) na Ngimila Ndombeji Mashana (27), wote wakazi wa Mbesi na wakulima.

Aidha, watu wawili walijeruhiwa katika tukio hilo ambao ni Manyanda Ramadhan Masasila (35) na Michael Aloyce Msanga (28). Majeruhi hao walikimbizwa hospitali kwa matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepuka madhara yanayoweza kusababisha majeraha au vifo, hususan kujikinga na maeneo hatarishi wakati wa radi.