Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limefanikiwa kuwafikisha mahakamani vijana saba kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kuzusha habari za uongo za kuibiwa nyeti katika eneo la Mbaroni, wilayani Sumbawanga.
Tukio hilo lilitokea Aprili 20, 2026, ambapo vijana hao wanadaiwa kumshambulia mwananchi mmoja kwa kumtuhumu kuhusika na wizi huo, hatua iliyosababisha maumivu kwa mhanga.
Akitoa taarifa hiyo, Polisi walisema vijana hao waliifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Ilemba ambapo walikabiliwa na mashitaka yanayowakabili.
Aprili 21, 2026, mahakama iliwatia hatiani vijana saba kati ya wanane waliokuwa wanashitakiwa na kuwahukumu kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Aidha, kila mmoja aliamriwa kulipa fidia ya shilingi laki moja kwa mhanga wa tukio hilo.
Majina ya waliotiwa hatiani ni Joseph Anania Bulaya (22), Meshack Daniel (21), Simon Vitalis (21), Dismas Gustave Kayumbe (22), Emmanuel Richard (24), Charles Juma (22) na Erasto Matondwa (19).
Katika hatua nyingine, mkazi wa kijiji cha Kambo, wilayani Kalambo, Bosco John Fatachi (38), anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kushambulia mtoto mdogo kwa kumtuhumu kuiba fedha kidogo, huku uchunguzi ukiendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limeonya wananchi kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.

Tunapatikana Kupitia