Watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga leo Mei 4, 2026 wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa Kidijitali unaotumika Kufuatilia, Kusimamia na Kukagua Matumizi ya Fedha za Serikali (Inspection and Finance Tracking Management Information System IFT-MIS), mfumo unaolenga kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi wa fedha za Serikali.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Bw. Nassir Kirusha amesema lengo kuu la mafunzo ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma kwa kuhakikisha miradi na matumizi ya fedha yanafanyika kwa kuzingatia viwango, ubora na weledi unaotakiwa.
Amesisitiza kuwa ufuatiliaji sahihi wa matumizi ya fedha za Serikali katika Ofisi za Umma ni msingi muhimu wa uwajibikaji, huku akibainisha kuwa uelewa mzuri wa matumizi ya mfumo wa IFT-MIS utasaidia watumishi kujibu hoja kupitia mfumo.
Kwa upande wake, muwezeshaji wa mafunzo hayo, Bw. Marwa Wankyo, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi Mkoa wa Rukwa amesema mfumo wa IFT-MIS umeundwa kusaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma, na hivyo kuchangia kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Wananchi.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya kidigitali ili kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali za umma na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa jamii.












Tunapatikana Kupitia