RUKWA - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, amewataka wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara Rukwa (RIBM) kuwa wabunifu, waadilifu na wenye nidhamu ili kuchangia maendeleo ya Taifa na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika Mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliyofanyika leo, Juni 11, 2026 mjini Sumbawanga, amesema vyuo vya kati vina mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wa kati, wabunifu na wajasiriamali watakaosukuma mbele uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu nchini.

Amesisitiza matumizi sahihi ya TEHAMA katika elimu na kuwataka wahitimu kutumia teknolojia kwa manufaa ya jamii huku wakizingatia maadili, uaminifu na nidhamu wanapoingia katika soko la ajira au kujiajiri.

Mahafali hayo yamewaleta pamoja wahitimu wa ngazi ya Astashahada na Stashahada katika fani mbalimbali na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi za elimu, viongozi wa dini, wazazi na wananchi wa Mkoa wa Rukwa.